
Katika kukabiliana na athari zinazoongezeka za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa vyanzo vya maji vinavyosababishwa na shughuli za kibinadamu, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia na Serikali ya Japan, imezindua rasmi Mradi wa Kuimarisha Mbinu za Asilia za Usimamizi wa Vyanzo vya Maji na Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi katika Bonde la Usangu, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya.
Mradi huu, unaotekelezwa na Bodi ya Maji Bonde la Rufiji chini ya Wizara ya Maji, unalenga kunufaisha zaidi ya wananchi 10,000 kutoka vijiji 45 vya Bonde la Usangu. Kupitia mradi huu, wananchi watawezeshwa kwa njia mbalimbali ikiwemo kuanzisha vikundi vya kiuchumi, kurejesha mito iliyoathirika, kuimarisha kilimo endelevu, na kudhibiti matumizi ya ardhi kwa njia endelevu ili kulinda vyanzo vya maji.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Nathan Belete,amesema kuwa dunia inakabiliwa na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi, na hivyo miradi kama huu wa Bonde la Usangu ni muhimu katika kukabiliana na athari hizo na kulinda ustawi wa watu na uchumi wa nchi.
Balozi wa Japan nchini Tanzania Yoichi Mikini ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Japan na Tanzania unalenga kusaidia juhudi za kulinda mazingira, ikiwemo kuhifadhi vyanzo vya maji ambavyo ni msingi wa maisha ya jamii nyingi nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji Dkt.George Lugomela amesema kuwa kupitia mradi huu, Serikali itaweza kurejesha mtiririko wa maji katika mito iliyopo ukanda wa juu wa Bonde la Usangu ambayo imeathiriwa na shughuli za kibinadamu zisizo endelevu.
Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Rufiji Mhandisi Florence Mahay amefafanua kuwa utekelezaji wa mradi huu unahusisha ushiriki wa wananchi kwa njia ya elimu, kampeni za upandaji miti, na udhibiti wa shughuli za kibinadamu karibu na vyanzo vya maji, ili kuhakikisha mradi unakuwa endelevu na wenye tija kwa muda mrefu.